/> MIAKA 58 YA KIFO CHA PRINCE LOUIS LUDOVICK RWAGASORE: MWASISI WA TAIFA ALIYEZIMWA NA MAADUI WA UKOMBOZI – Global Pan Africanism Network <
  • GA -3342821 Accra ,Ghana
  • +254700614290/+233541098521

MIAKA 58 YA KIFO CHA PRINCE LOUIS LUDOVICK RWAGASORE: MWASISI WA TAIFA ALIYEZIMWA NA MAADUI WA UKOMBOZI

MIAKA 58 YA KIFO CHA PRINCE LOUIS LUDOVICK RWAGASORE: MWASISI WA TAIFA ALIYEZIMWA NA MAADUI WA BHNa: Leonard Chakupewa Soza,

BUJUMBURA, BURUNDI.
13/10/2019.

 

 

 

 

Tarehe ya leo, 13/10/1961, majira ya mchana kwa saa za Afrika ya kati, taifa changa la Burundi wakati huo, lilizizima kwa simanzi na mshtuko mkali. Tukio lililotokea siku hiyo, ndilo kwa kiasi kikubwa lilikuwa kama kiini cha migogoro yote iliyofuatia baadae. Siku hiyo ikiwa salama, wakati wananchi wakiendelea kuungoja kwa hamu uhuru wao kutangazwa mwaka ambao ungefuatia, 1962, shujaa wao, Incungu yi gihugu (Mwasisi wa taifa) na Waziri mkuu mteule, Umuganwa au Mwana Mfalme Louis Ludovick Rwagasore, aliuawa kwa risasi. Ni tukio baya na la kuumiza, lililotokea eneo la hoteli ya Lake Tanganyika (Hotel du Lac Tanganyika), inayoelekeana na Ziwa Tanganyika, jijini Bujumbura, likiwahusisha watu wanne: Jean Kageorgis, Mgiriki kwa utaifa na asili, na raia wengine watatu wenyeji (Warundi). Wakati mauti yakimfika mwana mwema huyo, alikuwa akila mlo wa mchana hotelini hapo.

Maadhimisho ya kumbukizi yake kitaifa, yatafanyika nchini humo siku ya Jumatatu, tarehe 14/10/2019, kutokana na mwaka huu tarehe ya kifo chake kuangukia siku ya Jumapili. Shule zote na vyuo, ofisi za umma na taasisi zote za kiraia vitakuwa mapumzikoni ili kumuenzi shujaa huyu wa taifa, mjamaa kisera,aliyedhamiria kulikwamua taifa na kansa ya ukabila, kansa inayoendelea kulitafuna hata leo.

Alizaliwa Oktoba 10, 1932 akiwa uzao wa kwanza, mjini Gitega kwa Mfalme Mwambutsa Bangiricenge (WA NNE), na Malkia Therese Kayonza. Baba yake ndie alikuwa mfalme wa mwisho kabisa kutawala taifa hilo kama dola ya kifalme, kabla ya mfumo wa ufalme kupigwa marufuku mwaka 1966 na kiongozi wa kijeshi, Michel (Michael) Micombero. Mara baada ya kupata elimu yake Burundi, Rwanda na baadae nchini Ubelgiji, rasmi mwaka 1956 Mwana Mfalme alirejea nyumbani kuongoza vuguvugu la uhuru wa taifa, kinyume na mapendeleo ya familia yake akiwemo babaye, waliotaka asalie kama kiongozi ktk mlolongo wa ufalme asiyejihusisha na siasa ‘za vurugu’ Louis hakusikiliza, badala yake akasimama kidete kuwataka Wabelgiji kujiandaa kutoa uhuru wa taifa hilo.

Kwa kuamini kuwa ingekuwa njia rahisi ya kuwaleta pamoja wananchi wake kujadili masuala ya uhuru wao na kushikamana vema, Mwana Mfalme alianzisha vyama vya ushirika (cooperative unions) nchini mwote. Hata hivyo, muda mfupi baada ya kufanya hivyo, serikali ya kikoloni ilitoa tangazo la kuvipiga marufuku, tangazo lililobainisha wazi hatua kali za kuchukuliwa dhidi ya yeyote ambae angejaribu kuendelea kuviendesha au kuvihamasisha chini chini (underground). Marufuku hiyo haikumvunja moyo wala kumrejesha nyuma shujaa huyo, zaidi ya kumuimarisha zaidi na zaidi. Miaka miwili baadae, yeye na washirika wake wa karibu kama Pierre-Claver Ngendandumwe (muhutu wa kwanza kuchaguliwa Waziri mkuu baada ya kifo cha Mwana Mfalme Rwagasore) waliasisi chama cha Union for National Progress, UPRONA, (chama cha siasa kinachoendelea hata sasa nchini Burundi, na ndiko anakotoka Makamu wa kwanza wa rais, Bw. Gasto Sindimwo), alichokiongoza mwenyewe. Kupitia chama hicho, aliwaamuru wananchi kukataa kulipa kodi na tozo yoyote nyingine ya kikoloni, kama njia ya kuwadhoofisha ili watoe uhuru wa nchi. Pia, Mwana Mfalme aliitisha maandamano makubwa, ambayo yeye mwenyewe alishiriki huku akisisitiza kwamba, serikali waliyohitaji haikuwa ya kuchangia na Wabelgiji, bali ya wazalendo waliochaguliwa kwa uzingatiaji wa sheria na usawa wa jamii zote katika uwakilishi.

Mwaka 1960, uchaguzi ngazi ya wilaya zote za nchi ulifanyika, na chama cha Christian Democratic Party, PDC, kilichoungwa mkono na kupewa nguvu na serikali ya Ubelgiji kilishinda viti vingi dhidi ya kile cha kizalendo cha UPRONA. Hata hivyo, mambo yalibadilika mwaka 1961, kwenye uchaguzi ndani ya Bunge. Katika uchaguzi huo, UPRONA, chama cha kiongozi mzalendo Mwana Mfalme Louis Rwagasore kilijizolea takribani 75% ya viti vyote vya bunge. Rasmi akatangazwa kuwa ndie Waziri mkuu mteule aliyetakiwa kuiandaa nchi na kupokea uhuru wake mwaka 1962.

Wakati wananchi wakijiandaa kuupokea uhuru wao, na kumshangilia waziri mkuu wao wa kwanza mzalendo, kila kitu kilibadilika, pale shujaa huyo alipopigwa risasi na maadui wa ukombozi, uhuru na maendeleo ya taifa, watu waliopendelea ukoloni zaidi ya kujitawala. Watu waliopenda ukabila uendelee, kwa kuwa walinufaika zaidi na kujisikia salama. Watu walioamini katika ‘SISI’ na wengine kuwaita ‘WAO’ ndani ya taifa moja, lenye historia na utamaduni unaofanana.

Aliuawa kwa sababu alikataa yote hayo. Aliyakataa kwa maneno, aliyakataa kwa vitendo. Moja ya matendo yanayothibitisha kichefu chefu chake kwa ukabila, ni hatua yake ya kumuoa binti Maria Ntamikevyo, toka jamii ya Kihutu. Ifahamike kuwa, shujaa huyu alizaliwa katika familia ya Kitutsi. Hadi kufikia wakati huo, jamii hizi mbili zilishajengeana uhasama wa kutooana au kuhusiana kutokana na chuki zilizopandikizwa baina yao na wakoloni kwa muda mrefu. Mwana Mfalme alibaini kwamba kuwafunza watu kuwa ukabila haufai, ni muhimu kwanza wewe kuwa mfano. Alitaka wananchi waanze kuoana, kuheshimiana, kupendana kama jamaa moja ya WARUNDI, si kujipambanua kwa koo zao, pua zao, urefu au ufupi wao kama mkoloni alivyowafunza.

Jambo ambalo wengi hawafahamu ni kuwa, kiongozi huyo alikuwa swahiba wa karibu sana na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwasisi wa taifa la Tanganyika, lililojitwalia uhuru wake mwaka 1961 toka kwa Waingereza na miaka mitatu baadae, yaani 1964, kuungana na Zanzibar kuunda “TANZANIA” ya sasa. Inadaiwa kuwa kutokana na ukaribu wao ulioshamiri toka miaka ya hamsini mwishoni, mengi ya mambo aliyosimamia Mwana Mfalme, kupinga ukabila nchini mwake likiwemo, alishauriwa na Mwalimu. Tanzania, taifa aliloliongoza Mwalimu Nyerere licha ya kuwa na makabila zaidi ya 120 yanayozungumza lahaja tofauti tofauti, haijawahi kuingia katika vita wala mgogoro wowote kikabila.

Mwana mfalme Louis Ludovick Rwagasore kimwili, hatunae tena. Kiroho, kihekima na kibusara hata hivyo, hajawahi tuondokea. Kazi aliyoianza, imeendelea kusalia mfano na msingi mwema kwa uhuru wa taifa la Burundi, halikadhalika alama ya kujitambua, heshima na utu wa Mwafrika. Jukumu letu ni kuyaendeleza yote mema ambayo kwa dhati ya moyo wake aliyasimamia na, yaliyosababisha apoteze uhai wake.

Kwa miongo sasa nimeendelea kuamini kitu kimoja: kama Rwagasore angeendelea kuishi hadi siku ya uhuru na kuitawala Burundi kama Waziri mkuu na baadae rais, machafuko na mauaji yote yaliyojitokeza miaka ya sitini, sabini, themanini mpaka tisini, HAYANGETOKEA. Karibu kote barani Afrika, hasa kule kulikowahi kumbwa na migogoro, fukuto la hali hiyo lilichangiwa na mamlaka za juu. Kwa maana nyingine ni kwamba, kwa sababu shujaa huyu alichukia na kupiga vita sana mitanziko ya kikabila, kwa vyovyote vile hangeruhusu taifa kutumbukia ktk vita ya wenyewe kwa wenyewe na mauaji yenye kuchochewa na ukabila. Kama Mwalimu Nyerere au Kenneth Kaunda, angesimama kidete kuwaunganisha wahutu, watutsi na watwa kusalia jamii MOJA, inayotambulishwa na utamaduni, historia, utu na msingi mmoja. Kama Sam Nujoma au Thomas Sankara, angewahamasisha na kuwaleta pamoja raia wote kwa kigezo cha utaifa, kuijenga nchi yao kwa mikono yao, busara zao, elimu na maarifa yao. Alijua kuwa kabla ya ujio wa wakoloni, jamii zote tatu za taifa ziliishi kwa amani: watwa wakijikita ktk utengenezaji vyungu na mitungi mizuri, watutsi wakifuga ng’ombe huku wahutu wakiendeleza kilimo cha mazao mbalimbali. Alijua kuwa hakukuwa na uwezekano wa jamii moja kuwa juu ya nyingine kwa kuwa, zilitegemeana. Ndio maana alichagua KUUNGANISHA WATU, si KUWAGAWA.

Kama waafrika, tunapowaenzi viongozi kama hawa, tunapaswa kujisaili kwa kina na mapana. Tunaongozaje? Tunaongozanaje? Kama leo mashujaa hawa wangerejea juu ya dunia, wangetiwa moyo na namna tunavyowaongoza watu au wangeishia kusema ‘Dunia simama nishuke’? Kama leo wewe kiongozi ungefariki dunia, unadhani wananchi wako wangekukumbuka kwa lipi? Wangekuenzi kwa kiwango cha Mwana Mfalme Rwagasore, au Mwalimu J.K Nyerere, Chris Hani, Robert Sobukwe, Kwame Nkrumah, Thomas Sankara, Haile Selassie au Muammar Gaddafi? Au ungeishia na aibu za kina Jean-Bedel Bokassa, Mobutu Sese seko, Michel Micombero na Idd Amin? Je wewe mwananchi, unafanya nini kuisaidia nchi yako kujiweka katika uhuru na uimara zaidi kiuchumi, kiusalama, kihuduma nk? Tunalalamika tu, huku hatufanyi lolote kuzilinda na kuziimarisha nchi zetu, au tunafanya vyote viwili, au hakuna hata moja tufanyalo kati ya hayo mawili? Kila mmoja, kiongozi au raia wa mataifa yetu, anajua majibu yake.

Tutambue kuwa ukombozi wa Afrika si jukumu la mtu mmoja au kundi fulani dogo la watu pekee. Linapaswa kuwa mzigo unaotuelemea sote, pasi na kujali kabila, hali ya maisha, historia au kitu chochote cha kutupasua makundi makundi. Hakuna watu waliojikomboa makuchani mwa udhalimu aina yoyote kwa kuendeleza migawanyiko na mitanziko baina yao. Historia inaonesha kote ulimwenguni kuwa, waliochagua KUJA PAMOJA, ndio waliofanikisha kunia mamoja na kufanikisha mikakati yao. Kama haingekuwa ushirika na umoja wa makamanda wake, Jenerali George Washington hangeweza kuitoa USA makuchani mwa Waingereza. Kama haingekuwa umoja imara wa wana Haiti, Jenerali Toussaint Louverture hangefanikisha kuwafurusha Wafaransa na kuifanya Haiti kuwa taifa la kwanza la watumwa weusi kuundwa nje ya Afrika. Bila ushirikiano thabiti wa watu wake, Mwenyekiti Mao Tse Tung hangeweza kuing’oa serikali ya vibaraka wa Waingereza nchini China mwaka 1949. Ni ushirikiano baina ya wanyonge na masikini uliopelekea Wabolshe chini ya Vladimir Lenin kuifurusha madarakani serikali ya makabaila. Bila ushirikiano wa pamoja, hakuna taifa liwezalo.

Badala ya kukena meno kwa migawanyiko inayoendelea ndani ya mataifa yetu kwa misingi yoyote ya ovyo, tuipige vita kwa gharama zote. Ni kwa kufanya hivyo, tutawafanya mashujaa kama Mwana Mfalme, Incungu yi gihugu, Louis Ludovick Rwagasore kuendelea kupumzika kwa amani na enzi kwa kuwa hilo, miongoni mwa mengi mema na mazuri, ndilo alilohubiri na kusimamia hadi mwisho wa maisha yake juu ya ulimwengu.

Pumzika ktk kheri mwana mwema.

MUHIMU: Picha zilizoambatishwa ni kuhusu maisha yake: harakati zake, ndoa, kifo chake, mashtaka ya waliomuua na namna alivyopumzishwa.

Tags Cloud

#RIPJJRAWLINGSABMABM 2020ABMConferenceAddis AbabaAevis DugasAfricaAfrica DayAfrica my story challengeAfrican AmericanAfrican Business MonthAfrican ChildAfrican History ArchivesAfrican NarrativeAfrican UnionAfrican-AmericansAfricomAfrocentrismAgenda 2063Amat NdureAmilcar CabralAmy AshwoodApartheidAU AmbassadorAUC ChairpersonAUC Elections 2021AutomobilesBeesBenny WendaBlack ConsciousnessBlack HistoryBlack Mental HealthBlack UnityBootstrapBrazzavilleBuy Africa Build AfricaCalvin KleinsCape VerdeCaribbeanCharityChildren RightsChinaAfricaCivil RightsClimate ActionColonial AgreementsColonialismCommunityCongoCoupCOVID19CultureCyclingCyril RamaphosaDAC2020ConferenceDecolonizationDevelopmentDiasporaDisabilityDjiboutiDr Arikana ChihomboriEconomyEcowasEducationEgyptElectionsEnvironmentEthiopiaExploitationFacebookFijiFood SecurityForeign Military BasesForeign RelationsFranceFree MandabayanGarifunaGenocideGERDGhanaGhana ElectionsGlue AppGPANGuineaHead BallHistoriaHistoryHondurasHorn of AfricaHuman RightsIHEBAImperialismIndependenceIndigenous PeopleIndonesiaInequalitiesInvesting In AfricaIWritewhatilikeJacob ZumaJusticeKenyaKwame NkrumahKwame TureLeadershipLesothoLiteratureLobsterLumad PeopleMagufuliMaliMali EmpireMarxismMediaMelanesiaMilitarizationMotorcycleMugabe MemorialMy Hair My CrownMy StoryNatural ResourcesNatureNeocolonialismNGONigerNigeriaOral LiteraturePacificPan African ConferencePan AfricanismPatrice LumumbaPaul KagamePhilippinesPlightPNGPoliticsQRacismRobert MugabeRwandaSADCSahelScramble for AfricaSecuritySelf DeterminationSlaverySomaliaSonghaiSouth AfricaSportsSteve BikoSudanTanzaniaTanzania ElectionsTechnological AdvancementTechnologyThe Poor ManThomas SankaraTravel AdvisoryTribalismUgandaUhuru KenyattaUKULMWPUNUN Security CouncilUNGAUnited States of AfricaUnityUS War CrimesWangari MaathaiWest AfricaWest PapuaWest Papua UprisingWomen EmpowermentWordPressWorld Afro DayXenophobiaYouthZambiaZimbabweZindzi Mandela

Leave A Comment

× Whatsapp
%d bloggers like this: